Baadhi ya nguo za mitumba |
Na Mwandishi wetu.
Ninapo taja masoko makubwa ya nguo za ndani za mitumba, hapa nazungumzia Mwenge, Ilala, Tandika na hata Manzese.
Wanawake ndio watumiaji wa kubwa kwani kwa upande wa wanaume nguo zao kubwa za ndani ni kaoshi, soksi na taiti.
Lakini kwa upande wa wanaweke hupendelea zaidi kutumia sidiria, nguo za kulalia, taiti na hata chupi.
Nguo hizi za ndani za mtumba, hupendwa zaidi kwasababu baadhi husema ni imara na zina dumu lakini pia hupatikana kwa bei raisi sana, zingine huuzwa miatano au elfu moja na zipo za mpaka elfu kumi na zote ni za mtumba.
amoja na urahisi huo, watumiaji wanafahamu nini juu ya madhara ya kuvaa nguo hizi za ndani zilizo valiwa na watu wengine ambao hatuwajui? Hatujui afya zao na wala magonjwa ambayo huenda wanayo.
BBC imezungumza na baadhi ya watumiaji wa nguo hizo za ndani baadhi wanaonyesha kuto jua lolote kama yanaweza kuwepo madhara.
"Mi hayo madhara hata siyajui ila napata zangu nguo kwa bei poa na napendeza kama kawaida. Kama kuna madhara haya," anasema bi Aisha wa soko la karume".
Hata hivyo Ally Saleh mtumiaji wa nguo za ndani za mitumba anasema yeye huangalia zilizo mpya mpya.
"Mimi huwa nachukua ule mtumba wa grade A na zangu zinakuwa mpya mpya hazijatumika sana, ila kuhusu madhala labda zile zilizo chakaa kupita kiasi. Mie singlendi zangu ata boksa napata kali mtumbani," Ally anaiambia BBC.
Wengine wanafurahia ubora hali inayopelekea kufumbia macho juu ya elimu waliyo nayo.
"Mie naambiwa tu kwamba zina madhara lakini ukiziona zinaonekana bora na nzuri kuliko za dukani yaani ukivaa sidiria ya dukani inafanya matiti yanakuwa mama ni bebe, wakati ya mtumba kwa raha zangu kitu talk to me inakamata muruaa," Nola Almasi anaiambia BBC.
Hata hivyo kumekuwa na maoni mbali mbali juu ya madhara ya nguo za ndani za mitumba wengine husema zinaleta saratani, fangasi na baadhi huamini zinaharibu kizazi. Pamoja na yote yasemwayo baadhi yetu hufumbia macho na huamini kuwa ni propaganda za ushindani wa kibiashara.
Hata hivyo katika nguo hizo za ndani za mitumba zipo nyingi ambazo hazijatengenezwa kwa mali ghafi ya pamba, zimetengenezwa kwa polyista malighafi ambayo hainyonyi maji. Hali inayopelekea baadhi kupatwa na muwasho sehemu za siri.
Daktari Fredrick Mashili wa hospitali ya taifa Muhimbili ili kufahamu zaidi juu ya ukweli wa madhara ya nguo za ndani za mitumba.
"Kunakuwa na uwezekano wa kuwepo madhara kiafya na mara nyingi ni matatizo ya ngozi zaidi ndo yanaweza kusababishwa na hizo nguo, kutokana na ukweli kwamba huenda aliyekuwa anazitumia hizo nguo anatatizo flani la ngozi.
Kwa mfano ukiongelea vitu kama fangasi ambavyo vinauwezo wa kukaa kwenye mazingira magumu na kuishi kwa muda mrefu sana, kwa maana hiyo hata kama zilikuwa zimesafirishwa kwa muda fulanikwenye hali ya ukavu na nini bado kunakuwa na uwezekano wa kuwepo kwa vimelea au vitu fulani ambavyo ni sehemu ya fangasi ambavyo baadae mtu mwingine akivaa anauwezo wa kupata hilo tatizo," Daktari Mashili anaiambia BBC.
Hata hivyo daktari huyo anasisitiza kuwa upo uwezekano wa kuwepo kwa magojwa mengine ya ngozi ambayo haya sababishwi na fangasi na hii inategemea ni muda gani tangu nguo hizo zimetoka kwa mtumiaji wa awali na kuanza kutumiwa na mtumiaji wa sasa.
Daktari Mashili amesisitiza kuwa, kama kuna ulazima wa kuzitumia nguo za ndani za mitumba ni vyema mtu akazisafisha na dawa zile kali ambazo zinaweza kusaidia kuuwa viji dudu kuliko kufua tu kawaida na kisha kuivaa.
Tangu mwaka 2009, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), lilipiga marufuku uuzaji wa nguo za ndani za mitumba na kutoa kipindi cha ukomo kwa wafanyabiashara wa bidhaa hizo. Baada ya kipindi cha mpito kuisha, TBS walifanya maamuzi ya kukamata na kuchoma nguo hizo za ndani za mitumba ili kutekeleza agizo la sheria ya mwaka 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani zilizokwishatumika.
Hata hivyo harakati hizo hazikufua dafu kwani mpaka sasa nguo za mitumba bado zipo katika takribani kila soko la nguo za mitumba Tanzania.
Kutoka BBC Swahili