Na Adimu Nihuka Jr.
Ingawa kuna wanaowahi au kuchelewa kidogo, kwa kawaida wasichana huanza kuona damu ya
hedhi kwa mara ya kwanza wanapofikia umri kati ya miaka 12 na 16. Hali hii ni
muhimu katika maisha na makuzi ya msichana, hujulikana kama kuvunja ungo.
Msichana
anapovunja ungo, anatazamiwa kuendelea kupata damu ya hedhi kila mwezi hadi
anapofikia kipindi cha kukoma hedhi. Katika sehemu mbalimbali duniani, wanawake
wengi hufikia kipindi cha kukoma hedhi wakiwa na umri kati ya miaka 45 na 55,
lakini wapo wachche wanaofikia kipindi hicho wakiwa na miaka 60 au zaidi.
Utafiti
uliofanywa na Rosemary Mrina mwaka 2009 mkoani Singida ulibainisha kuwa
wanawake wengi hapa nchini hufikia kipindi cha komahedhi wakiwa na wastani wa
miaka 47. Komahedhi ni hali ya kawaida ya utendaji wa mwili wa mwanamke
inayotekea mwanamke anapopoteza uwezo wa kuzaa kutokana na kuwa na umri mkubwa.
Dalili
ya kwanza inayoonyesha kuwa mwanamke amefikia komahedhi ni kutokuona damu ya
hedhi kila mwezi kwa zaidi ya miezi 12 mfulululizo. Mwanamke anapofikia hali
hii hawezi kupata damu ya hedhi. Katika hali ya kawaida siyo rahisi msichana
mwenye afya njema kukoma hedhi katika kipindi cha ujana. Lakini jambo la
kushangaza ni kwamba, baadhi ya wasichana huingia mapema katika kipindi cha
komahedhi wakiwa na umri kati ya miaka 13 na 19 na wanawake wengine huingia
kipindi hicho wakiwa na umri chini ya miaka 40.
MATATIZO YA KOMAHEDHI.
Katika
ulimwengu wa leo ambao unasisitiza wasichana kupata elimu darasani hadi kufikia
chuo kikuu, kuna uwezekano mkubwa kwa baadhi ya wasichana na wanawake wanotumia
muda mwingi kutafuta elimu, kujikuta wanakoma kupata hedhi katika kipindi cha
kuhangaika kupata elimu. Hali ya komahedhi ya mapema huwanyima baadhi ya
wasichana na wanawake fursa ya kupata watoto na kufurahia maisha ya ndoa zao.
Halikadhalika,
wasichana na wanawake wengi wanaopata hali hii wanakabiliwa na athari hasa za
kisaikolojia na wakati mwinginw huangukia katika imani za kishirikina kwa
kuhisi kuwa wamerogwa. Mbali na dalili za kutokuna damu ya mwezi, msichana pia
anaweza kutokwa na jasho mara kwa mara wakati wa usiku, kukosa usingizi na
kukojoa mara kwa mara.
Pia
kupungua kwa hamu ya tendo la kujamiiana, kupungua kwa majimaji yanayolainisha
uke wakati wa tendo la kujamiiana, ukavu wa ngozi na kukasirika bila sababu za
msingi. Mambo haya huongeza hali ya msongo wa kumnyima msichana furaha na raha.
Watafiti
wengi wa masuala ya afya ya uzazi wanabainisha kuwa kutokana na sababu
mbalimbali, akti ya asilimia moja hadi 4% ya wanawake walioko katika umri wa
kuzaa hukabiliwa na tataizo hili la komahedhi ya mapema. Huko nchini marekani
4% ya wanawake hupata hali hii.
Pia
utafiti uliofanya na taasisi ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi (ISEC)
iliyoko Bangalore, India nao wamebaini kuwa, wastani wa 8% ya wanawake wenye
umri kati ya miaka 35 na 39 wanapata komahedhi ya mapema kuliko walivyotarajia.
Tatizo
hili linaweza kusababishwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, tiba ya
upasuaji ya kuondoa mfumo wa kizazi, tezi za mayai, matibabu ya kutumia miozi
yz jua, dawa za kutibu saratani, athari ya baadhi ya kemikali au urithi wa
vinasaba vyenye mwelekeo wa tatizo hili.
KINACHOSABABISHA KOMAHEDHI
Takwimu
zinaonyesha kuwa kati ya 10% na 20% ya wasichana na wanawake wote wanaopata
tatizo hili, ni wale ambao katika familia zao kuna historia ya kutokea kwa
komahedhi ya mapema. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na wanasayansi chuo
kikuu cha California San Frncisco (UCSF) cha Marekani na kuchapishwa mwaka 2013
katika jarida la Cancer, ulibainisha kuwa uhusiano wa karibu akti ya urithi na
vinasaba ya BRCA na kutokea kwa komahedhi ya mapema.
“Matokeo
ya utafiti wetu yanaonyesha kuwa mabadiliko yaliyotokea katika vinasaba hivi
yana uhusiano wa kutokea kwa mapema hali ya komahedhi, hali ambayo inaweza
kusababisha ongezeko la hali ya ugumba”, anasema Dr Mitchell Rosen, Profesa wa
sayansi ya uzazi na magonjwa ya wanawake, Chuo kikuu cha California San
Francisco.
Mambo
mengine yanayochangia kutokea kwa komahedhi ya mapema ni tezi ya mayai
kushindwa kutengeneza mayai na kuzalisha vichocheo vinavyodumisha hali ya
jinsia ya kike, lishe duni, matumizi holela ya dawa kama vile Tamoxifen,
uvutaji mkubwa wa sigara, magonjwa ya tezi za shingo pamojana na kisukari.
Vyanzo vingine ni uambukizo wa virus vya mafindofindo, ugonjwa wa kifua kikuu
pamoja na msongo wa mawazo wa muda mrefu.
Wasichana
wanaofanya mazoezi mazito ya kukimbia pia wanaweza kupata hali hii.
Kuhusuvyanzo vya tatizo hili Dk Marjorie Dixon, bingwa wa tiba za uwezeshaji
wanawake wagumba kupata watoto katika kituo cha sayansi za afya cha Sunnybrook
kilichopo jijini Toronto nchini Canada anasema:- Mara nyingi sababu hazieleweki
ila baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa kutokana na kupungua kwa vichocheo vya
jinsi mwili hasa Estogeni.
WENYE TATIZO
WAFANYE NINI?
Msichana
anayepata komahedhi ya mapema, anashauriwa kuonana na mtaalamu wa magonjwa ya
wanawake haraka ili kufanyiwa tiba pamoja na uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja
na kuchunguza afya yake kuhusu uwezekano wa kuwa na tatizo la kisukari au
maradhi ya tezishingo. Ili kupunguza athari mabay za hali hii inashuriwa
kuboresha hali ya lishe kwa kutumia vyakula vyenye vitamin na madini kwa wingi.
Matumizi
ya maharage ya soya au mazao yake pia yanasaidia kwa vile yana dawalishe aina
ya Phytoestrogens kwa wingi ambayo yanasaidia kudumisha afya ya jinsi kwa
wanawake wa rika zote. Mazoezi mepesi kila siku pia yanaaidia kupunguza athari
mbaya ya tatizo hili kwa wasichana na wanawake kwa ujumla.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi la
tarehe 21/11/2015.
No comments:
Post a Comment