Sunday, November 26, 2017

TAHADHARI WATOTO WANAOTUMIA TEHAMA

Na Adimu S. Nihuka Jr. (Kijana anayechipukia kwa kasi katika masuala ya TEHAMA, KIUMA Tunduru- Ruvuma)

K
umekuwa na malalamiko mengi kuhusu watoto kuharibikiwa wanapotumia au kuangalia vifaa mbalimbali vya teknolojia kama vile simu au kompyuta. Kwanza tukubaliane jambo moja kwa upande wa runinga (TV), wazazi au walezi wengi hawajui matumizi sahihi ya vifaa walivyonavyo kwa ajili ya kutumia wao wenyewe au watoto wao. Unaponunua vifaa vya runinga hasa hivi ving’amuzi utakuta ina sehemu imeandikwa parent guide au mwongozo kwa wazazi.

Huu ni mwongozo wa wazazi au mlezi kuhusu kifaa chake kama anaangalia na mtoto au atamwachia mtoto pale utaweza kuweka nywila (password) kwenye baadhi ya vipindi ili mtoto asiweze kuangalia au kuchuja baadhi ya maudhui ambayo ni mabaya kwa mtoto.
Suala la parent guide lipo pia kwenye kompyuta; hii ni program ya bure ingawa ziko zinazouzwa zenye mambo mengi zaidi lakini nyingi ni bure kabisa hapa unaweza kuingia kwenye simu au kompyuta na kuweka taratibu ambazo mtoto atafuata ili aweze kutumia kifaa chake vizuri na kama akiingia sehemu ambayo sio sahihi haiendi au itamuondoa kabisa.
Kuna wazazi wanaowaacha watoto wao kununua filamu zozote wanazotaka wenyewe. Katika makasha ya filamu nyingi kwa nyuma utakuta wameandika maudhui ya filamu yenyewe, lugha zilizomo, vipande vya mapenzi au mauaji na umri wa mtu anayetakiwa kuangalia kama ni kuanzia miaka 13 au 18 au wote na saa nyingine mpaka jinsia. Kama mzazi siku unaweza kufanya msako kwenye kabati ambayo mtoto wako anahifadhi filamu zake, angalia kama zinaendana na umri wake.

Angalia nyuma ya kasha ingawa wengine wanaweza kuwa wanahifadhi kwenye kompyuta zao, laikini unaweza kufuatilia kwa njia ya mtandao kupata maelezo ya filamu husika. Kwa hali ilivyo sasa, nashauri wazazi kuendesha misako hii kwa kuwa vijana wengi wameathiriwa na filamu hizi. Usipozikuta kabatini basi ziko kwenye kompyuta.
Wakati mwingine unakuta mzazi ana simu yake ya kisasa amejiunga kwenye mitandao kadhaa ya kijamii na kujiunga kwenye makundi au sehemu za kupokea habari mbalimbali. Humo unaweza kupokea picha chafu au zinazo tisha na vingine ambavyo sio sahihi kwa mtoto wake ashike, achezee anavyotaka na mtoto huyo ataweza kuingia na kuona vile vitu baba au mama yake anavyoangalia au kupokea.

Pia kuna suala la kuzingatia vitu watoto wetu wanavyofundishwa shuleni kama vipindi vya kompyuta tuangalie kwa karibu wanafundishwa nini hasa kama walimu wenyewe wana uelewa kuhusu masuala wanayofundisha. Mwisho ni kazi ya serikali na wizara ya elimu kuhusu suala hili. Kwa kipindi kirefu tumeona filamu za Kiswahili zikitoka huko nje ya nchi hasa filamu za kihindi, kikorea, n.k zikiwa na masuala mengi yaliyo kinyume na maadili. Hizi filamu huuzwa kama njugu mitaani zikikosa maelezo ya maudhui yaliyomo na umri wa watu wanaopewa kuzitazama.
Ni vizuri wizara ya elimu ikabadili baadhi ya mitaala yake ili iendane na wakati wa sasa ambapo kuna ukuaji mkubwa wa sayansi na teknolojia pamoja na upashaji wa habari. Vitu hivi watoto wakianza kufundishwa mapema, vitasaidia kujua vibaya na vizuri na kuvitumia kwa faida zaidi vile vizuri na kuachana na vibaya.
Kwa upande wa mitandao hasa wamiliki, waanze kuweka vitu vya ndani ya nchi zaidi vinavyojenga uzalendo na hamu ya watu hasa vijana kujifunza na kuangalia masuala ya ndani ya nchi badala ya kuwekea wasome vitu visivyoendana na tamaduni zetu.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment