KUHUSU ZIWA TANGANYIKA...
Hili ni miongoni mwa maziwa makubwa na mashuhuri Afrika na Duniani kwa ujumla.
Ziwa Tanganyika linapatikana Magharibi mwa Tanzania likipakana na nchi za Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.
Sifa za Kipekee;
Ziwa Tanganyika ni la kwanza kwa urefu Duniani (the first longest lake in the world) likiwa na umbali wa kilometa 673 kutoka ncha ya Kaskazini iliyoko Bujumbura nchini Burundi hadi ncha ya kusini iliyoko Mpulungu nchini Zambia na upana wa wastani wa kilometa 50.
Ziwa Tanganyika ni la Pili kwa kina kirefu Duniani (the second deepest lake in the world) likiwa na kina cha mita 1470 likitanguliwa na Ziwa Baikal lililopo katika milima ya Siberia nchini Urusi katika mpaka wa kaskazini na Mongolia.
Ziwa Tanganyika lina ujazo mkubwa wa maji baridi (fresh water) Duniani likiwa na ujazo wa kilometa za ujazo 18,900 km³ ambazo ni sawa na 17% ya maji yote baridi duniani.
Ziwa Tanganyika lina Hifadhi mbili za Taifa katika fukwe zake za Gombe na Mahale ambazo ndizo Hifadhi pekee nchini Tanzania wanakopatikana wanyama aina ya Sokwe-mtu (Chimpanzee) wanaoishi katika mazingira yao ya asili milimani.
Ziwa Tanganyika lina zaidi ya aina 350 za samaki na wengi hupatikana katika ziwa hili tu ikiwemo mamia ya aina za samaki wa mapambo.
Ni ndani ya Ziwa Tanganyika ndiko ambako inapatikana meli kongwe zaidi ya abiria Duniani ambayo inahudumu mpaka sasa na kuingizwa katika kitabu cha kumbukumbu za Dunia (Guinness World Book of Records) ikiwa na miaka zaidi ya 100. MV Liemba (Graf Goetzen) iliundwa nchini Ujerumani mwaka 1913 na imekuwa ikihudumu mpaka leo baina ya bandari za Kigoma (Tanzania), Kalemie (DRC) na Mpulungu (Zambia)
Miji mikubwa katika Ziwa Tanganyika ni mji Mkuu wa Bujumbura nchini Burundi, mji wa Kigoma Ujiji nchini Tanzania, mji wa Kalemie nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na mji wa Mpulungu nchini Zambia.
Jina la ziwa hili "Tanganyika" (i.e the great lake spreading out like a plain) ndilo mwaka 1919 baada ya Ujerumani kushindwa vita Kuu ya ya Dunia (1914-1918) na kupokwa koloni lake la Afrika Mashariki (Deustcheost afrika) ndilo jina lililotumika kuliita koloni lililowekwa chini ya uangalizi wa Uingereza la Tanganyika ambalo baada ya kujipatia Uhuru wake Desemba 9, 1961 lilizaa Taifa la Tanganyika na baadae 1964 Jamuhuri ya Tanganyika na Jamuhuri ya watu wa Zanzibar ziliungana na kuzaliwa Taifa la TANZANIA ya leo.
Ukibahatika kutembelea Magharibi mwa Tanzania basi usiache kulitembelea Ziwa Tanganyika na kushuhudia mengi mazuri na ya kuvutia.
Karibu Tanzania.
Karibu SwahiliKwetu Tours
No comments:
Post a Comment